Skip to main content

MR & MRS MWAKATWILA | JIFUNZE NAMNA YA KUULINDA MOYO WAKO (AU NAFSI) NA KUUTOA KWENYE MAANGAMIZO SEHEMU YA 22

23
0

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Ninamshukuru Mungu ambaye ametupa nafasi hii ya kukuletea somo darasani. Kumbuka Tuna somo refu kidogo lenye kichwa.

 

JIFUNZE NAMNA YA KUULINDA MOYO  WAKO (AU NAFSI) NA KUUTOA KWENYE MAANGAMIZO.

 

Na neno lililobeba ujumbe mzima ni hili."Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.  Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."(Mithali 4:20-23).

 

Na nichukue nafasi hii kuwashukuru watu wote mliotutumia shuhuda zenu namna Mungu atendavyo kazi baada ya kujifunza somo hili darasani. Tumepokea shuhuda za ajabu sana kutoka kwa wanadarasa mbalimbali. Unajua tunapopokea shuhuda hizo nasi tunajengwa na kupata msukumo mkubwa wa kuwaletea masomo. Kumbuka mwalimu yoyote hupenda kuona kama darasa linaelewa, na si kuelewa tu pia kuona kile kinachofundishwa kimeleta matokeo gani.

Kwa hiyo tunapozipokea shuhuda zenu  tunabarikiwa na tunamrudishia Roho Mtakatifu utukufu na heshima zake.

Pia nichukue nafasi hii kukuomba ebu omba kwa Mungu atupe chakula cha kiroho kilicho cha wakati baada ya kumaliza somo hili. Naona moyoni mwangu Kukushirikisha hili kwani somo hili tulililojifunza kwa sehemu hii tuliyopewa naenda kumaliza siku si nyingi. Kwahiyo omba kwa Mungu atupe somo jingine la kutoka patakatifu pake.

Ebu basi tuanze kujifunza. Katika kipindi kilichopita tulijifunza eneo lile la  Jifunze kuomba kwa roho au kunena kwa lugha kwa muda mrefu ili uijenge nafsi yako.

Leo nataka nikuonyeshe jambo lingine ambalo unatakiwa ulijue katika eneo hilihili la maombi yako ya kuijenga nafsi au moyo wako nalo ni hili.

 

JIFUNZE KUOMBA MUNGU AIACHILIE DAMU YA BWANA YESU KRISTO MOYONI MWAKO KILA MARA

Unaposoma maandiko utaona damu ya Bwana Yesu Kristo ndani yake imebeba mambo mengi mno mno. Bahati mbaya watoto wa Mungu wengi tunaifahamu Damu hii kwa sehemu ndogo.  Moja ya kazi iliyomo ndani ya damu ya Bwana Yesu Kristo ni hii ya kuijenga na kuipatia uhai nafsi ya mtu.

Ngoja niseme kwa mtindo huu. Unaposoma maandiko utaona damu iwe ya mnyama au ya mtu ina uhai.  Maandiko yanasema hivi. " Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote.Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu.  Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu."(Mwanzo 9:3-6).

 

Ukiipitia hiyo mistari utagundua damu ndani ya maandiko inaitwa uhai. Angalia hapo  neno linasema "Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka;" uhai wetu umewekwa ndani ya damu. Sikia uhai wa mwili wako umo ndani ya damu.  Na maandiko yanatuonyesha nguvu iliyomo ndani ya damu ni yaa ajabu mno.

 

Angalia mfano. Kaini alipomuua Habili damu ya Habili ndiyo iliyomshitaki Kaini. Angalia mistari hii uone." BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.  Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;"(Mwanzo 4:9-11).

 

Damu ya Habili ndiyo iliyolia kutoka ndani ya kinywa cha aridhi na Mungu aliisikia kabisaa. Mungu hasemi Kaini nimemsikia Habili akinililia. Anasema nimeisikia sauti ya damu ya ndugu yako inanililia. Ohoo!! Kumbe damu inaweza kutoa sauti kabisaa. Kama unafikiri nakutania muombe Mungu leo akusikizishe leo sauti mbalimbali katika ulimwengu wa roho. Utashangaa kusikia sauti nyingi za damu zilizomwagwa na watu furani zikilia.

 

Zingine zinalilia mataifa furani ambayo ndiyo yalihusika kuzimwaga, zingine zinalilia watu furani au makabila furani au jamaa furani yaani ukoo nk. Wayahudi siku ile wana msulibisha Bwana Yesu walimwambia Pilato  damu yake iwe juu yetu na watoto wetu. Unajua walikua wanamaanisha nini? Walikuwa wanamaanisha damu hiyo kama wameimwaga pasipo haki basi iwalilie wao na watoto wao.

 

Ndiyo maana nakwambia damu inaweza kulilia kuanzia mtu aliyeimwaga mpaka watoto wake. Ngoja nikupe mfano huu wa ajabu sana. Angalia mistari hii." Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki."(Luka 11:49-51).

 

Ukiipitia hiyo mistari utaona nguvu ya damu inavyoweza kufuatilia kizazi na kizazi cha mtu aliyeimwaga. Utaona wazi kuwa damu ya Habili  iliendelea kulia mbele za Mungu. Na Bwana Yesu aliwaambia kitu hicho hao ndugu ambao walikua hawafahamu kuwa kuna damu wanadaiwa mikononi mwao na walitakiwa wailipe. Bwana Yesu aliwaambia damu hiyo inatakwa katika kizazi chao. SIKIA DAMU YA HABILI!! Ukijiuliza utaona hao ndugu hawakuwepo siku ile Kaini anamuua Habili.

 

Damu pia ilichaguliwa na Mungu kuwa ndiyo inatakiwa ishughulikie nafsi au mioyo ya watu iliyoharibika. Kumbuka tulikotoka nilikufundisha kuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa nafsi za watu ni dhambi. dhambi inapofanywa na mtu inaupotezea moyo nguvu ya uzima wake.

 Sasa ilikuuludishia moyo au nafsi yako uzima na uhai wake unaweza kutumia damu ya Yesu Kristo ambayo ndani yake imebeba uhai wa mtu na uzima. Sikia  Mungu aliichagua damu tokea agano la kale ili iwezekushughulikia nafsi zile zilizopoteza uhai au uzima.

 

Mungu aliwaagiza watu watoe sadaka maalumu za wanyama au ndege iliichukuliwe damu  kwa kazi maalumu, na aliagiza ziletwe madhabahu na sadaka hizo  zichinjwe na damu ya wanyama ifanye kazi ya kushughulikia nafsi au mioyo ya watu hao. Maandiko yanasema hivi. Angalia mistari hii."  Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu."(Mambo ya Walawi 17:10-12).

 

Mungu alipoona mioyo au nafsi za wanadamu zimeharibiwa na dhambi na lazima ufahamu wazi kuwa moyo wako ukiharibiwa kwa shambulio la aina yoyote ile ushirika wako na Mungu huvunjika. Ngoja nikupe  mfano, Kaini alipomuua Habili, ushirika wake na Mungu ulivunjika. Msikilize Kaini asemavyo. " Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua."(Mwanzo 4:13-14)

Kaini alipofanya hiyo dhambi tu akajikuta ameachana na Mungu. Anasema wazi kuwa amesitika mbali na uso wa Mungu. Na kitendo hicho Kaini anasema ni adhabu kubwa mno. Ngoja nikwambia kama kunakitu unatakiwa uhakikishe unatafuta katika maisha yako yote ni hiki HAKIKISHA USO WA MUNGU UNAKWENDA NA WEWE POPOTE PALE.

Wana wa Israeli walipoabudu sanamu tu Mungu alimwambia Musa hivi." BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri."(Kutoka 32:7-8).

 

Kitendo cha hao ndugu kuabudu miungu mingine tu kiliharibu nafsi zao. Musa aliwaombea msamaha kwa Mungu na  Mungu alikubali. Lakini ukisoma maandiko utaona kuwa Ingawa Mungu aliwasamehe lakini Mungu aliuondoa uso wake kwa hao ndugu. Yaani ushirika wa Mungu na hao ndugu haukuwepo. maandiko yanasema hivi.

 

Musa akaenda tena kule juu mlimani kumwomba Bwana Mungu aurudishe tena uso wake uende na wana wa Israeli.  Angalia mistari hii uone."BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii;nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri.............Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa.Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako."(Kutoka 33:1-4 na 8-18).

 

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kuwa dhambi ile ya kuabudu sanamu au miungu ilimuondoa Mungu katikati ya wana wa Israeli. Mungu akapanga malaika ndiye aende nao huko Kanani. Wana wa Israeli pamoja na Musa waligundua kuwa hiyo ni habari mbaya kwelikweli.

 

Unajua walilia na kuomba uso wake usiondoke. Nampenda Musa aligoma kuondoka na malaika akamwambia Mungu haujaniambia ninani ntakaeenda naye baada ya kumwambia odoka na watu hawa. Si kua Musa hakuambiwa na Mungu kuwa atatakiwa aambatane na malaika. Musa akajifanya hana habari hiyo. Unajua Mungu aliwasamehe wana wa Israeli kabisa kuwa hatawaua ila aliondoa uwepo wake nao.

 

Mungu ili apate nafasi ya kukaa na hao ndugu waliojiharibu nafsi zao aliamua kutengeneza utaratibu  maalumu wa kuitumia damu ili iwe inafanya kazi ya kuwapatanisha hao ndugu na Mungu. Damu ilifanya kazi ya kuzitakasa hizo nafsi za hao watu na kuzipatanisha na Mungu.

Neno kutakasa maana yake kutenganisha au kuondoa uchafu na kitu halisia. Ndani ya kutakasa kuna kujenga au kupata sura ya kitu kizuri( kukarabati).

Sasa kitu kimojawapo leo hii kinachoweza kuwa sehemu ya ujenzi wa nafsi yako au moyo wako ni DAMU YA YESU KRISTO. Damu ya Yesu Kristo inaweza kunena kabisaa kama ile damu ya Habili. Lakini kuna utofauti kati ya damu ya Habili na damu ya Bwana  Yesu Kristo, damu ya Yesu yenyewe  inanena mema maandiko yanasema hivi."Na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habil"(Waebrania 12:24).

Damu hii ndiyo tuliyopewa katika agano hili jipya. Unaweza kuitumia damu hii kukupatanisha nafsi yako na Mungu kama unaona huko nafsini mwako  hakuja kaa sawa na uso wa Mungu umeondoka kwako. Usi kubari kuona uso huo unakuondokea kisa tu umejiharibu nafsini mwako kwa dhambi furani. Kumbuka kitendo cha kuhifadhi hasira au wivu au chuki,husuda, au tamaa mbaya  kulipa kisasi, uizi uongo, uzushi kutokumpenda Mungu, kutokua mvumilivu, ukiwa mtu mgomvi nk ni dhambi.

Na Mungu akiona moyoni mwako  upo hivyo fahamu uso wake unaweza kuondoka kwako.  Sasa jifunze kukimbilia kwenye hiyo damu ili UJENGWE MOYONI MWAKO HUKO. Itafute  hiyo damu kwa njia ya maombi ili ije kujenga Nafsi au moyo wako  si kutakasa tu. ITAKE PIA  ILI IJE NA  IJENGE NAFSI YAKO ILIYOBOMOKA

Ebu tufuatane katika kipindi kijacho tutaendelea kuona damu hii inavyo weza kukujenga nafsini mwako.

Mungu akubariki sana.

Na: Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila

admin