Skip to main content

MR & MRS MWAKATWILA | JIFUNZE NAMNA YA KUULINDA MOYO WAKO (AU NAFSI) NA KUUTOA KWENYE MAANGAMIZO SEHEMU YA 20

19
0

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana.

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Kabla sijakuletea somo leo hili nilikua na mambo mawili nilitaka kukushirikisha. Kwanza ninawashukuru watu wote mlionitakia heri ya siku ya kuzaliwa kwangu. Mungu awabariki sana. Asante kwa maombi yenu na faraja yenu kwetu. Tunahitaji maombi yenu sana, msikome kutuombea kwa Mungu.

 

Jambo la pili ninapenda kukupa taarifa kuwa Tarehe 5-12-3-2017. Tutakua na semina pale Betheli Sae Kkkt. Tutaanza saa tisa mpaka saa kumi na mbili na nusu. Upatapo taarifa hii mjulishe na mwenzio. Ombea semina hii ili kile Mungu amekikusudia kukifanya kifanyike sawasawa na kusudi lake.  Baada ya kukupa hayo mambo mawili nikukaribishe sasa tuanze kujifunza.Katika kipindi kilichopita nilikufundisha nguvu ya kinywa chako inavyoweza kutumika katika kuiponya au kuihuisha nafsi yako au ya mtu mwingine.  Ebu tusogeembele kidogo katika kona hiyo.  Siku moja nilikua naongea na mtu mmoja  alikua ni mwanamke, unajua nilishangaa Roho Mtakatifu aliniambia ndani yangu. Aliniambi hivi ONGEA VIZURI NA HUYU MTU KWASABABU MOYO WAKE UMEJERUHIWA TOKEA ZAMANI ONGEA NAYE KWA MANENO YA FARAJA.

 

Unajua niligundua siku hiyo kuwa katika kinywa cha mtu kuna nguvu ya kuiponya nafsi ya mtu aliyejeruhiwa tokea zamani. Unajua baada ya kuambiwa hivyo nilijipanga katika kusema kwangu. Unajua kuna watu waliojeruhiwa moyoni utawaona ni watu ambao hawaelewi haraka, hawana kumbukumbu, wengine hawajiamini kabisaa, wamejikatia tamaa na hisia zao zimepigwa hazi hisi kupendwa kuthaminiwa na watu na hata na Mungu.

 

Sasa unapokutana na mtu huyo nakwambia ukweli ukikosea katika mfumo wa kuongea naye tu, utakua unamjeruhi au kuiangamiza nafsi yake kabisaa. Unajua unapokua mtumishi unatakiwa uwe makini sana kwenye eneo hili la namna ya kutumia kinywa chako katika kusema na watu.

 

Unajua mtu ambaye Mungu aliniambia niwemwangalifu katika kuzungumza naye ni mtu aliyeokoka na ni mtumishi kabisaaa. Ni rahisi kumuona kuwa ni mzima kiimani nk. Kumbe tokea mtoto kajeruhiwa moyoni na Mungu akaniambia anajeraha moyoni nijue namna ya kuongea naye. Mtu huyo nikwambie hawezi kukaa na watu wengine bila kukwaruzana naye.

 

Watu wengi wanamuona jeuli mkali na kiburi. Kumbe ni mtu mzuri ila mgonjwa, nilipokaa naye niligundua aliaharibiwa tokea mtoto yaani akiwa binti tu. Alilelewa na mama wa kambo, alikutana na magumu mnooo tokea mtoto. Unajua unapokutana na mtu wa namna hiyo hapendi hata kufundishwa. Si anaona kama unamsimanga vile?

 

Sasa unapotaka kumfundisha lazima maneno yako yawe mazuri,ukikosea tu namna ya kuzungumza naye  ni rahisi kusema huyu ndugu anakiburi hataki kufundishika. Kumbe mwenzenu alianza kuumizwa na kitu kufundishwa toka kwa mama wa kambo. Unajua kanisa linahitaji huduma ya kichungaji kuliko vile tuwazavyo.

 

Maandiko yanasema hivi." BWANA ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake."(Zaburi 23:1-3). Kazi ya mchungaji mojawapo ya mchungaji ni hii ya kuhuisha mioyo ya watu iliyojeruhiwa kwelikweli.

 

Unaweza kusema ataihuisha kivipi? Kwa kuwaombea na kwa namna anavyoongea nao. Watu wengi hawajui kuwa kitu kimoja wapo kitumikacho  kuhuisha nafsi ya mtu au kuiangamiza ni kinywa. Mtumishi yoyote yule lazima ajue kuwa kwa kupitia kinywa chake anaweza kuhuisha nafsi za watu wengi sana na kwa kupitia kinywa hichohicho anaweza kuziangamia nafsi nyingi mno.

 

Moja ya somo muhimu ambalo Roho Mtakatifu atashughulika na mtumishi wake aliye muita ni kumfundisha kwenye eneo la KUZUNGUMZA KWAKE. Biblia inasema hivi. "Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu."(Wakolosai 4:6).

 

 Angalia mistari hii pia"Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake."(2Timotheo 2:24-26).

 

Maneno yako yana nguvu mno katika kuhuisha hata nafsi za wenye dhambi. Unajua ni rahisi kusema huyu mtumishi ana injili nyepesi mno ila watu wanamfuata sana ana roho nyingine huyo!!! Watu humfuta mchungaji au mtumishi anayewa huisha moyoni. Wakigundua tu, hawabanduki huko hata ufanyeje au uwaambieje. 

 

Ukiona watu wanaokoka na wanakimbia eneo lile waliokokea au wanaludi kukeee walikotoka fahamu mfumo uliopo hapo hauna nguvu ya kuhuisha mioyo yao. NA HILI NI TATIZO KUBWA MNO KATIKA KANISA LA MUNGU.

 

Umewahi fikiri kwanini kulikua na utofauti wa huduma ya Bwana zyesu na makuhani na hao mafarisayo? Angalia VINYWA VYAO VILIKUWAJE. Kulikua na utofauti mkubwa mnoo.

 

Unajua leo hii ukimtazama Bwana Yesu Kristo utaona kinywa chake kilijaa maneno yaliyokolea munyu mno. Hata tabiri uliotabiliwa juu yake unasema hivi. "Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao; kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na BWANA, ili atukuzwe."(Isaya 61:1-3).

 

Maneno hayo alikuja kuyadhibitisha alipokuja angalia mistari hii. "Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu."(Luka 4:16-21).

 

Bwana Yesu Kristo alifanya kazi kubwa mno ya kuhuisha mioyo ya watu iliyoumizwa iwe na dhambi au mazingira waliokulia nk. Yaani aliwahurumia sana watu aliangaika kuwapa hata chakula, aliwaponya magonjwa yao bila kuwasimanga weeee!! au kuwatisha nk. Fikiria kidogo Bwana alisha kutana na wagonjwa ambao alijua kabisaa wametenda dhambi akawaponya kwanza ndipo akawaambia msiludie kutenda dhambi tena.

 

Kinywa chake kilijaa maneno yakuhuisha mno. Wewe soma habari zake zote ndiyo utajua injili ya Bwana Yesu ilikuaje. Injili ni habari. Sasa angalia namna hiyo habari kinywani inatokaje. Ni ngumu kunielewa hasa kwa wale waliofikiri maneno mimi naita magumu ndiyo yanamfanya mtu aache dhambi.  Unaweza kusema imeandikwa kemea au onya. Ni kweli kabisaa. Sasa tatizo lipo kwenye uelewa wa maneno hayo kwa watu wengi sana.

 

Kuonya au kumemea si kuhukumu na kuvunja moyo. Unaweza onya hata kukemea kwa kufundisha  mtu kabisaa. Ninachotaka kukufundisha ni hiki angalia sana neno HILI UNAPOZUNGUMZA NA MTU UNAMFARIJI UNAMHUISHA AU UNAMFANYA ATIWE FURAHA? Kuna watu utasika wanasema mimi sijaitwa niwafurahishe watu!!

 

Mmhh sina maana umfurahishe mtu kwenye eneo la kutenda dhambi, sina maana hiyo. Hata kama anafanya dhambi fikiria anakifungo cha uovu nafsini. Yaani tokea anazaliwa yeye ameeona Mungu wako si Mungu kwake, unafikiri KUMPIGIA KELELE KUTAISAIDIA NAFSI HIYO KUMKUBALI MUNGU WAKO?

 

Mimi nakwambia kuna watu walianza kuzini tokea watoto. Niliwahi kutana na mtu mmoja aliniambia alianza kuzini akiwa mdogo kabisaaa. Anasema alikua anawaona dada zake wakienda kwa wanaume furani wanazini, yeye akiangalia, akakua na yeye akawa akiambatana nao hao ndugu zake na akawa anazini na yeye. Ilifika alikua anazini nahao dada zake na aliona ni kitu cha kawaida tu. Akiwa mtu mzima akasikia neno uzinzi hakujua uzinzi nini alipoambiwa hakuamini kuwa jambo hilo ni dhambi.

 

Kisa aliona watu wa familia yake wafanyavyo tokea utoto. Nafsi ya huyo mtu iliharibiwa tokea zamanii. Akawa mzinzi mno. Nafsi yake ilihalibiwa tokea zamani mnoo. Sasa iliuiponye hiyo nafsi lazima uhakikishe maneno yako yanakaa sawasawa.

 

Ni ngumu kunielewa lakini wewe tembea humu duniani ndiyo utajua wewe uonavho ni dhambi kunawatu hawanaufahamu kabisaa kuwa hicho ni dhambi. Fikiria kuna maeneo uchawi ni sehemu ya maisha yao sasa unapokwenda kwa watu walioumizwa nafsini mwao kwa dhambi ya uchawi ambayo ndani yake inaibada ya miungu. Usifikilie utakua na hayo maneno yako magumu ndiyo watakuelewa eti. Eheee!!  Niliwahi kwenda eneo furani yaani watu wa huko wanaukarimu wakupitilizia. Anakuachia mpaka mke. Ndiyo walivyo. Nilishangaa sana.

 

Tulipofika kule mwenyeji wetu aliyetupeleka akatushitua kuwa mkiona mwanaume anawaondokea nyumba msilale humo ndani. Mwambieni alale tu mkewe. Bahati nzuri sisi hatukufanyiwa hivyo.. Unajua hao watu ni Wakristo. Wamezaliwa hivy wako hivy. Lugha yako ya kuongea nao lazima ikolee munyu hasa nakwambia. Nilipoanza kufundisha nilimuomba Mungu anipe kinywa cha kueleweka. Walinielewa

 

Watu wengi wanafunga na kuomba sana. Lakini huwa hawayaoni matokeo ya maombi yao. Unajua ni kwanini?  Angalia mistari hii utaona jibu hapo" (Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA?Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui."(Isaya 57:6-11)

 

Nilitaka hapo uyaone hasa maneno haya."na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; "Ukiiangalia hiyo njaa si njaa ya chakula ni njaa ya KUHITAJI UHUISHO MOYONI. Kunawatu nafsi zao zimeteswa na dhambi tokea utotoni kabisaa.

 

Sasa sikia nafsi yako wewe inatakiwa ikunjuke ili iihuishe nafsi ya mtu aliyeteswa moyoni. Mungu anasema jambo hilo ni mojawapo ya mambo ayatakayo ayaone kwa mtu afungaye na kumuomba  ili amjibu maombi yake.

 

Sasa fuatilia waombaji wengi uone midomoni mwao wanatoa nini pale wazungumzapo na watu. Wengi wanamaneno magumu sana. Yaani ni laumuweee, kuhukumu wee, masimango wee, manung'uniko wee nk. Sikia badilika kabisaa kinywani mwako ili Mungu akujibu maombi yako mpendwa.

 

Pia jifunze kuisemesha nafsi yako kama sehemu ya tiba. Ukiona moyoni mwako kuna shambulio lililokupata na unataka kuiponya basi unaweza tumia kinywa chako kuzungumza na moyo au nafsi yako . Angalia mfano huu uone hiki nikwambiacho.

 

Angalia mistari hii "Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu. Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.  ....,,Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu."(Zaburi 42:5-6 na ule wa 11).

 

Mfalme Daudi alipogundua kuwa ndani yake yaani moyoni au nafsini hakuko sawa aliamua kuisemesha hiyo nafsi yake ili ikae sawa. Au ili aiponye nafsi yake ilimbidi aiisemesha.. Angalia Akaiuliza swali kwanini imeinama? Na alipojua kilichoiinamisha akaiambia KWA KINYWA CHAKE ISIINAME!!

 

Unaweza kuiambia hata nafsi ya mtu mwingine au yakwako kabisaa na ikasikia. Kama leo hii unaona umeshambuliwa na shetani moyoni na kukuondolea furaha jifunze kuisemesha hiyo nafsi kuwa haitakiwi ibebe huzuni. Unaweza sema nayo na kuiamuru kabisaa ifanye kile wewe unataka ifanye na itatii.

 

Kama unaona unakosa ujasiri yaani roho ya hofu imekujaa, au umepoteza hali ya kujiamini na upo dhaifu  jifunze kuisemesha maneno kama  haya. "Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari."(Yoeli 3:10).

 

Maandiko yanasema aliye dhaifu na Aseme mimi ni hodari!!! Hata kama wewe unaona kuna hali ya kushikwa kwenye tamaa ya uzinzi, Isemeshe nafsi yako kuwa MIMI SI MZINZI!!! Kinywa kinatumika kuumbia tabia furani. Sasa ukisema mimi si masikini wakati nafsi imezungushiwa ngome za kukuonyesha wewe huna kitu na masikini ndiyo upinyaji wa akili zako na hisia zako hizo zikukandamizazo kwa kukuonyesha kuwa wewe huna kitu.

 

Ukiona dada moyoni unajikatia tamaa ya kuolewa badilisha hiyo hali kwa kutumia kinywa chako. Iambie nafsi yako kwanini kuinama? Wewe ni bonge la mwanamke hajatokea bado wa kukufaa. Iambie Yupi anakuja wala usiiname UTAMUONA MUNGU EE NAFSI YANGU!! Utaona moyoni kila kitu kinaanza kukaa sawa sawa!!! Ile hali ya kuumia inaondoka hali ya furaha na kujiamini inaludi. Baada ya siku si nyingi Mungu ataumba yale uliyoyasema. Cha msingi yaseme kwa Imani. Yaani uwe na uhakika na kile usemacho.

 

 Unaweza kutumia kinywa kuliondoa pigo la nafsini kwa kusema kwako tu. Adui au watu wakisema utakufa na moyo wako ukakidaka hicho kilichosemwa wewe kiondoe kwa kuisemesha hiyo nafsi yako maneno kama haya. Kwanini kuinama eee  nafsi yangu?  Sintakufa bali ntaishi ili niyasimulie matendo makuu ya Mungu!!!!

 

Jifunze kuiponya hiyo nafsi yako kwa kutumia kinywa chako. Mungu akubariki sana.

 

Na: Mr Steven Mrs Beth Mwakatwila

admin