Skip to main content

MR & MRS MWAKATWILA | JIFUNZE NAMNA YA KUULINDA MOYO WAKO (AU NAFSI) NA KUUTOA KWENYE MAANGAMIZO SEHEMU YA 17

15
0

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Ninakukaribisha tena katika darasani ili tujifunze. Katika kipindi kilichopita nilikufundisha kuomba kwa Mungu ili akuhuishe nafsi yako. Na amini umeanza kuyaweka haya kwenye matendo. Sikia haitakua vizuri usome weeee masomo haya na usipoyaweka kwenye matendo ni hasara kabisaa.

 

Leo nataka tujifunze jambo lingine ilitupate kuiponya na kuilinda mioyo yetu.Kumbuka maandiko yanasema hivi. "Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."(Mithali 4:20-23).

 

Ebu tuliangalie jambo lingine unalotakiwa ulifanye ili uuitoe moyo wako kwenye maangamizo nalo ni hili.

 

JIFUNZE KULIWEKA NENO LA MUNGU MOYONI MWAKO.

 

Angalia mistari hii uone hiki ninacho kuambia."Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako."(Zaburi 119:25). Ukiitazama mistari hiyo utagundua kuwa mfalme Daudi aliomba kwa Mungu amhuishe nafsi yake sawasawa na neno la Mungu.

 

Mfalme Daudi alijua kuwa kuna jambo linalotakiwa lifuate baada ya kuomba kuhuishwa kwake. Nalo lilikua ni neno la Mungu. Sikia ili moyo wako uwe na uhai na uzima unahitaji neno la Mungu huko moyoni mwako. Sikia ili uitoe kwenye maangamizo hiyo nafsi yao au moyo wako lazima uhakikishe UNAOMBA UHUISHWE SAWASAWA NA NENO LA MUNGU.

 

Ngoja nikupe mfano huu. Mungu anapotuagiza kuwa tuilinde mioyo yetu alisema kuwa kama tutazisikia kauli zake hapo ndipo tutakua na uhai Ebu msikilize asemavyo. . "Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."(Mithali 4:20-23).

 

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa ndani ya neno la Mungu hapo kaita kauli ndiko kwenye uhai. Neno nafsi kwa lugha nyingine inaitwa pumzi hai. Sasa sikia kitu cha ajabu, Ili wewe upate uhai lazima ujifunze kulisikia neno la Mungu ambalo ndilo linaloleta uhai. Nafsi yako ikipigwa na kupoteza uhai wake na uzima ili ifufuliwe au iponywe itahitaji UHAI YAANI NENO LA MUNGU.

 

Mfano, Ikiwa hisia zako za upendo zimepigwa na zikabeba chuki ili kuziponya hizo hisia ni lazima upokee neno la Mungu linalokutaka wewe uwe na upendo. Hapo unatakia uilishe nafsi yako maneno kama haya."Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi....Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana."(Yohana 15:12 na 17). Angalia na hii."Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu;"(1Petro3:8)

 

Ngoja nikuongezee mingine kwasababu nataka ujaze neno la Mungu moyoni mwako sana." Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria."(Warumi 13:8). Ujaze na mstari huu moyoni mwako naamini utakua dawa nzuri sana moyoni mwako UKIJIVIKA

"Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu."(Wakolosai 3:12-14)

Ukiona hisia zako huko moyoni zimebeba chuki na unatakiwa usiikemee tu hiyo chuki. NENDA KWENYE NENO LA MUNGU NDILO PEKEE LITAKALO IHUISHA HIYO NAFSI YAKO ILIYOKUFA KUTOKANA NA CHUKI. Soma Neno la Mungu, ipitie hiyo mistari iwaze hiyo, ifikiri hiyo, itafakari hiyo UTAPATA AKILI AU UJUZI WA NINI WEWE UNATAKIWA UFANYE NI KUTOKUTUNZA CHUKI MOYONI . Hapo utakua salama moyoni mwako. NA USISHANGAE MAISHA YAKO YOTE HUTAKUA MTU WA KUTUNZA CHUKI MOYONI MWAKO

 

Naludia kukufundisha lisome hilo neno. Usiseme nililisoma. Sikiliza Huwezi tegemea dawa ya malaria uliyokunywa mwaka jana ikuponye na malaria uliyokutana nayo leo. Kama umekutana na malaria leo unatakiwa utafute dawa leo ili uinywe na uwauwe wale wadudu waletao homa ya malaria na kupelekea mtu kupoteza uhai na uzima mwilini. Hata kwenye nafsi ni hivyo hivyo. Kama kuna ugonjwa uitwao chuki, hasira, uongo mawazo mabaya nk. Ili uiponye hiyo nafsi au moyo unatakiwa uhakikishe unatafuta dawa ya nafsi Inaitwa neno la Mungu.

 

Sikia kama nafsi imebeba jeraha la chuki. Usitafute Neno tofauti na tatizo ulilonalo. Ngoja nikuulize swali. Unaendaje kunywa dawa ya ugonjwa wa macho wakati unaumwa malaria? Si utakufa hapo? Mioyo ya watu wengi leo hii imekufa kisa ni hiki hiki cha kukimbilia neno na kulijaza mioyoni lisilo wafaa kutokana na kukosa matatizo waliyonayo moyoni.

 

Wewe huna tatizo la uchoyo ni mkarimu mzuri unatafutaje maneno yahusuyo ukarimu? Tatizo lako si ukarimu tatizo lako ni hofu au woga, katafute mistari ndani ya Biblia inayozungumzia woga au hofu.

 

Ngoja nikupe huu mfano utaona kwanini watu wengi mioyo yao iko vile vile haibadiliki. Angalia mistari hii." Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi."(Yakobo 5:13).

 

Angalia watu wengi hawajui kuwa kama mioyo yao imepatikana na mabaya wanatakiwa waombe. Na kama imechangamka waimbe. Watu wengi hawajui namna ya kuilinda mioyo yao kwa kutumia kuimba tu. Maandiko yanasema moyo wako ukiwa na furaha au umechangamka unatakiwa uimbe. Kwanini tuimbe? Tunaimba ili KUUTUNZA UZIMA WA MOYO!!! Nisehemu ya ulinzi wa moyo wako na NDANI YA NYIMBO KUNAUHUISHO WA AJABU MNO HATUJUI TU.

 

Unaweza kuniuliza sasa naimbaje wakati nipo mahali kelele hazitakiwi? Sikia Mtu anaweza fanya mambo yake hukohuko ndani ya moyo wake hata watu wa huku nje wasijue mtu anafanya nini!!! Imba hivyo mahali ambapo sauti haitakiwi. Mungu anasikia kabisaa kuwa furani kaimba leo.

 

Mtu yoyote anayejua kumwimbia Mungu sifa akiwa na furaha akili zake na hisia zake na utashi wake HUJENGWA VIZURI. Wafuatilie waimbaji. Hapo sasa sizungumzii waimbaji watakao fedha au kuburudisha watu makanisani. Nazungumzia waimbaji wale wanaojitambua wao nikinanani na wamepewa kuimba kwa ajili ya nani. Waimbaji wa namna hiyo utawaona wana uwezo mkubwa wa kufikiri. Yaani mioyo yao iko salama.

 

Mungu anasema ukipatikana na mabaya huko moyoni mwako uombe. Angalia kama wengi huwa wanaomba. Hata wakiomba angalia wengi hawakai kwenye nafasi ya muombaji mpeleka mahitaji yake kwa Mungu. Wengi hukaa kwenye nafasi ya Mungu yaani wanahukumu, badara ya kumuachia mwenye nafasi ambaye ni Munguatoe hukumu. Utaona wengi wanashitaki badara ya kumuachia mwenye nafasi hiyo ya kushitaki ambaye ni shetani.

 

Kasome maandiko utaona mwenye nafasi hiyo ya kushitaki ni shetani anaitwa mshitaki. Sasa watu wengi wakijeruhiwa huko mioyoni, wakikimbilia kwa Mungu utaona wanafanya kazi ya kushitaki watu weee na kuwahukumu hao watu waliowajeruhi weee!!!

 

Kumbe wangeomba wapinywe mioyo yao bila kushitaki na kutoa hukumu Mungu angeishughulikia mioyo yao kwa kuiludishia uzima na uhai kabisaa.Jikague wewe mwenyewe utagundua mara nyingi wewe ni muasi, yaani UNAKALIA KITI CHA HUKUMU WAKATI SI CHAKO WEWE NI MUASI MPINGUA SEREKALI YA MBINGUNI. Ukiwa mshitaki fahamu unatumika na shetani Mungu hawezi kukupenda kabisaaa!!! Yaani wewe na pepo mnatofautiana kidogo tu. wewe ni mtu yeye ni pepo ila kwenye utendaji kazi mko sawasawa kabisa.

Sasa angalia ukifurahi unaimba nyimbo gani pia? Watu wengi wanaimba nyimbo za mipasho wanasema watu weee, ni nyimbo lakini ukizisikiliza wala hazimsifu Mungu ila ni maombi tuuuuu!!!! Aani Mungu atusidie.Zingine ni nyimbo za kutiana moyo sisi kwa sisi. Nyimbo kama hizo wakati furani zinajenga mioyo iliyokufa. Hata kwako inaweza kukutia moyo. Sasa lazima uangalie unaimba wimbo uliobeba nini. Siyo kujiimbia kisa ni wimbo wa Kikristo

 

Ngoja nikuulize swali unatatizo gani moyoni mwako Ni uchungu,? Ni hofu na woga? Ninini kimeinuka na kuibana akili yako? Unajua dawa ya vitu hivyo vyote ni nini? Ni neno la Mungu. Neno la Mungu lina nguvu mno kama litasomwa kwa faida. Ninavyosema kwa faida namaana hii. USILISOME KAMA HADITHI. Liko hai, linaweza kuumba tabia kabisaaa, linaweza ponya na kubadilisha mtazamo wa mtu kabisaaa.

 

Unaweza litafuta kama tiba moyoni mwako, Maandiko yanasema lina uhai. Angalia mistari hii. "Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo."(Waebrania 4:12).

 

Neno la Mungu lina uhai na nguvu na ukali kama upanga ukatao kuwili sehemu nyingine maandiko yanasema ni kali kama moto." Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?(Yeremia 23:29).

 

Kama neno la Mungu katika ulimwengu wa roho ni kali kama moto na lina makali kama upanga ukatao kuwili ebu Fikiri ulijaze moyoni mwako. Si utakua umejiwekea ulinzi mkubwa mno? Si utakua umejizungushia MOTO NA PANGA HUKO MOYONI? Nani atapenya? Sijui unanielewa? Unataka kuweka ukuta wa moto moyoni mwako? Badi jaza neno la Mungu. Unataka uwe na upanga mkali ulindao moyo? Upanga huo ni neno la Mungu, maandiko yana sema upanga wa Roho ni neno la Mungu. UNAPOANZA KUSOMA LEO NENO JENGA IMANI HIYO KUWA UNAWEKA MAPANGA HUKO NA UZIO WA MOTO HUKO MOYONI

 

Sikia nikwambie Penda kujaza neno la Mungu ndani yako kuliko kitu chochote. Unajua watu wengi wanapenda kuomba sanaaa. Ni vizuri. Lakini sikia uhai na uzima upo kwenye neno la Mungu. Ndiyo maana anasema mtu ataishi kwa neno la Mungu. Hasemi mtu ataishi kwa maombi. Napenda kuomba sana. Lakini najua uhuisho wa moyo na roho yenyewe upo kwenye neno. Kwa hiyo ntaomba Mungu niuhuishe nafsi yangu NA NIANAJUA ATAKACHOKIFANYA NIKIMUOMBA MAOMBI YA UHUISHO WA NAFSI YANGU. Atafanya hivi

 

Mungu yeye atakachofanya ni kunisukuma mimi nianze kusoma na kulisikiliza neno lake AMBALO NDILO LIHUISHALO MIOYO. Ngoja nikufundishe kitu. Ukianza kuomba maombi ya kumruhusu Mungu achunguze moyo wako na ukaingia ndani zaidi kuomba Mungu aihuishe nafsi yako fahamu Mungu atakachofanya ni KUKULETEA NGUVU YA WEWE UANZE KUPENDA KUSOMA NA KULISIKIA NA KULIELEWA NENO LAKE.

 

Wewe anza yale maombi. Utaona utaanza kupelekwa kwenye neno la Mungu. Usishangae unafungua Biblia unakutana na mistari inayokuelezea tatizo lako kabisaaa. Na kwakua umeomba uhuishwe nafsi mwako utashangaa utashi wako utaanza kufanya maamuzi ya kulitendea kazi neno la Mungu hata kama mwili hautaki.

 

Ndiyo hapo unashangaa unamsamehe na kumpenda mtu uliyekua unamchukia. Utashangaa akili zako zitaanza kuwaza vema na utapanga mipango na utashi wako utaanza kukusukuma kwenda kuiweka kwenye matendo hiyo mipango yako nk.

 

Naamini leo hii umepokea kitu darasani.

 

Mungu akubariki sana.

 

Na: Mrs Steven & Beth Mwakatwila

admin